Wasomi, wanasiasa wamuunga mkono Magufuli

WASOMI, wanasiasa, na wafanyabiashara waunga mkono juhudi za serikali za kupambana na wizi, udanganyifu na ukiukwaji wa sheria na taratibu kwenye sekta ya madini nchini na kutaka mfumo ubadilishwe ili dhuluma kwenye sekta hiyo na sekta nyingine ikomeshwe.

Maoni hayo ya wadau yamekuja baada ya taarifa ya uchunguzi wa biashara ya madini ya almasi na tanzanite uliofanywa na Kamati mbili zilizoundwa na Bunge, kuwasilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa Rais John Magufuli jana Ikulu jijini Dar es Salaam. Kutokana na taarifa hizo za Kamati za Bunge, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema matatizo hayo kwenye sekta ya madini nchini hayatokani na matatizo ya kisheria wala kisera, bali ni ukosefu wa ufuatiliaji, umakini na uwajibikaji kwa watu waliopewa dhamana ya uongozi wa kusimamia sekta hiyo.

Profesa Bana alisema Tanzania ina sheria na sera nzuri ikilinganishwa na nchi nyingine zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini pia ina wasomi wazuri wenye uelewa wa kutosha wa kupima na kuelewa mambo sentensi kwa sentensi na aya kwa aya, lakini tatizo lao ni kukosa uwajibikaji, umakini na ufuatiliaji. Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesigwa Baregu aliunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kwa kusema kuwa uzalendo wa kirasilimali ndiyo unaotakiwa kama ilivyokuwa nchini Venezuela.

Profesa Baregu alisema kuwa ni muhimu kwa taifa kujua mazingira ya mikataba iliyoingiwa kwa kuwa suala hilo limekuwa likipigiwa kelele na wabunge kwa zaidi ya miaka 10. Alisema njia pekee ya kuondokana na wizi na mikataba mibovu ni kuzingatia misingi na miiko ya uongozi kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja alisema hatua ya kuwasimamisha watendaji waliohusika na udanganyifu kwenye sekta ya madini haitoshi, bali mfumo wa kisheria na kanuni unapaswa kubadilishwa ili usitoe tena mianya kwa watu kufanya udanganyifu.

Aidha, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Augustine Mrema amesema Rais Magufuli ni kiongozi makini aliyedhamiria kuiletea Tanzania maendeleo makubwa kwa haraka katika kipindi chake cha uongozi, hivyo anapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.

Mrema alisema wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alijitahidi mno kupigania sekta ya madini na aliwahi kukamata dhahabu nyingi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ) mwaka 1991. Alisema dhahabu hiyo iliyokuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 170, ilikuwa imefungwa kiufundi kwenye vifurushi 12 kama miche ya sabuni na ilikuwa inatoroshwa kwenda Uarabuni.

Comments