Jeshi la Uganda laomba radhi


Jeshi la Uganda limeomba msamaha ambao ni nadra sana kutokea baada ya askari wake kuonekana kwenye mkanda wa video wakimpiga mwandishi wa habari ambaye alikuwa akitimiza wajibu wake kwenye maandamano ya kushutumu kukamatwa kwa mbunge Bobi Wine mnamo Jumatatu .Katika tukio hilo waandishi wengine nao walipigwa walipokuwa wakiarifu jamii juu ya maandamano hayo kupitia vyombo vyao vya habari.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi, ilieleza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na askari wake kuwa si cha weledi na kusema kuwa watakamatwa kwa muujibu wa sheria za jeshi nchini humo.

Kumekuwa na mvutano wa kisiasa nchini Uganda baada ya mbunge Bobi, na wabunge wanne wa upinzani, kukamatwa wiki iliyopita.

Bobi ni maarufu nchini Uganda awali kutokana na kujihusisha na tasnia ya muziki kabla ya kuchaguliwa kama mbunge mwaka jana, amefanikiwa kuteka umaa wa wana Uganda miongoni mwao vijana, na kuendesha harakati za kisiasa dhidi ya raisi Yoweri Kaguta Museveni anaarifu mwandishi wa BBC aliyeko mjini Kampala Catherine Byaruhanga.

Vijana wengi walioko sasa nchini Uganda walikuwa hawajazaliwa wakati raisi Museveni alipotwaa madaraka mnamo mwaka 1986.

Mapema wiki hii chama cha kutetea haki za binaadamu kilichoko mjini New York, kimewataka polisi na jeshi nchini Uganda kusitisha mara moja mashambulizi yao dhidi ya vyombo vya habari na waandishi habari nchini humo na kuheshimu haki za waandamanaji.

Katika video iliyorushwa mtandaoni, mwandishi wa habari wa shirika la Reuters James Akena, anaonekana akipigwa kwa fimbo na askari wawili mtaani katika mji mkuu, wa Kampala.

Kipigo kiliendelea kumuangukia mwandishi Akena hata alipoamua kusalimu amri na kuweka mikono yake juu huku akiwa amepiga magoti.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu linasema kupigwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari ni ushahidi tosha kuwa wa mamlaka nchini Uganda wanataka kuficha mwenendo wa vikosi vya usalama nchini humo.Katika taarifa yake, Jeshi limejitetea kuwa awali lina uhusiano mzuri baina yake na vyombo vya habari nchini humo.

Mbunge Bobi, ambaye jina lake kamili ni Robert Kyagulanyi, bado anaendelea kusalia kizuizini na kwamba anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya kijeshi siku ya Alhamisi kujibu mashtaka ya umili wa silaha kinyume cha sheria.

Familia ya mbunge huyo inadai kuwa alishambuliwa vikali, lakini jeshi, ambalo linamshikilia Mbunge huyo , limekana vikali madai hayo.

Naye raisi Yoweri Museven amekanusha taarifa kuwa Bobi Wine ameumia na kwamba ana majeraha mabaya, na kuziita taarifa hizo kuwa ni habari za kupikwa.

Comments