Wanaofanya biashara ya ngono kufikiwa na kampeni ya upimaji ukimwi


Na Ferdinand Shayo,Kilimanjaro.

Serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi imeanza mpango maalumu wa kuyafikia makundi maalumu kupitia kampeni ya upimaji wa Afya na kuanza matibabu ambayo inatarajia kuyafikia makundi maalumu ikiwemo Wanawake wanaofanya biashara ya ngono ili kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi .

Aidha huduma za mkoba zimeanza kutolewa kwa makundi hayo maalumu ambayo yako mbali na vituo vya afya ili kuwasaidia kujua hali yao na kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuanza matibabu pale wanapogundua kuwa wana maambukizi  hayo.

Kampeni ya kitaifa ya kupima afya kwa hiari kwa makundi maalum katika jamii mkoani kilimanjaro italishirikisha kundi la wanawake wanaofanya biashara ya ngono ambalo linaonekana limesahaliwa sana huku likikabiliwa na vitendo vya unyanyasaji na kuambukizwa virusi vya ukimwi.

Meneja wa Mradi wa Sauti unaofadhiliwa na shirika la kimataifa la misaada la Marekani (USAID) kanda ya kaskazini   Aminiel Mongi amesema, mradi huo umefanikiwa kuwapima watu 60,220 wa kundi hilo kati ya 75,000 waliotarajiwa mkoani kilimanjaro kati ya mwezi oktoba mwaka jana na juni mwaka huu.

Mongi amesema hayo katika uzinduzi wa kamati  ambayo itajihusisha na kampeni hiyo ya  "furaha yangu-pima,jitambue,ishi" mkoani kilimanjaro na kwamba kundi hilo pia linapewa elimu ya kujiepusha na vitendo wanavyofanyiwa ikiwemo kutishiwa maisha  na kubakwa.

Mganga Mkuu Mkoani Kilimanjaro Dr. Best Magoma amesema, kuzinduliwa kwa kamati hiyo ni utekelezaji wa agizo la waziri mkuu la kuitaka mikoa yote kuendesha kampeni hiyo baada ya kuzindua kamati ya kitaifa hivi karibuni.

Akizindua kamati hiyo kwa niaba ya katibu tawala wa mkoa huo katibu tawala msaidizi  Grace Makiluli amesema, makundi yote katika jamii hayana budi kushirikishwa katika kampeni hiyo wakiwemo watu wenye ulemavu

Comments